Ramon Umashankar alizaliwa katika tabaka ya juu ya Kihindu (Brahmin). Wakubwa wake kwa umri walimfundisha akiwa na umri ndogo ya kwamba yeye alikuwa mungu, na ya kwamba ili kuufikia uungu wake ni lazima afanye mazoezi ya yoga na kutafakari. Yeye kama kijana mbichi [tineja], Ramon alianza kushangaa kama kweli angempata Mungu kupitia kwa sanamu zile mbali mbali zilizoabudiwa katika mahekalu ya Kihindu [Kibaniani].
Ramon akaanza kuichunguza Biblia na madai ya Kristo. Yeye alikuwa amemheshimu Yesu siku zote kwa unyenyekevu wake aliokuwa nao, lakini sasa Ramon akasikia kwamba huyo Yesu alidai kwamba alikuwa ndiye Mwana pekee wa Mungu. Tena aligundua kwamba Wakristo wengi walionekana wanayo amani ambayo kutafakari kwa miaka mingi kulikuwa kumeshindwa kuifikia. Lakini, Ramon bado alikuwa amedhamiria kuipata kweli katika dini yake ya Kibaniani.
Lakini baadaye aliiona filamu iliyoonyesha maisha yake Kristo. Kwa mara yake ya kwanza alitambua kwamba Yesu alikuwa amepatikana na mateso na hofu kama mwanadamu. Kabla ya hapo alikuwa amedhani kwamba Yesu kwa njia fulani alikuwa ametumia uweza wake wa Uungu kuyakwepa maumivu yale yaliyotokana na kusulubiwa kwake. Lakini sasa, alishindwa kueleza habari za msalaba ule. Alishangaaa na kujiuliza-uliza: Hivi ilikuwa-kuwaje huyo Yesu aliweza kuyapitia mateso makubwa kama yale - kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi?
Ramon alipoendelea kutafakari juu ya kifo cha Kristo, alizidiwa nguvu kwa kudhihrishwa kwa upendo kama ule. Aliamua kukitupilia mbali cheo chake kinachotamaniwa sana na watu wa Brahmini [tabaka la juu la Kibaniani] na kutoa maisha yake kwa Yesu, Mwokozi wake. Alipoyalinganisha mambo yote na ule upendo wa kujitoa mhanga wa Kristo, Ramon alisema hivi, "Kila kitu cho chote kingine kikasambaratika."
Mbrahmini huyo kijana alikigundua kiini cha ile kweli ya Ukristo: yaani, Yesu Mwokozi wa ulimwengu.
