Kanisa Lilianzishwa Na Yesu
Maisha na mafundisho ya Yesu yalianzisha umoja wa imani na ushirika wa karibu sana katika kanisa lile la mitume walilolianzisha. Mitume wale walikuwa na uhusiano wa karibu kabisa na Kristo yule aliyefufuka. Paulo alitoa picha ya kifungo hicho cha karibu sana na kukilinganisha na uhusiano wa ndoa
“"Naliwaposea Mume mmoja, yaani, Kristo, ili niwalete ninyi kwake mkiwa bikira safi."”
Kulingana na maneno ya Paulo, kanisa la Kikrsto ni mwanamke safi, ni bibi-arusi wa Kristo, ishara inayofaa kabisa kwa kanisa lake Kristo alipendalo. Katika Agano la Kale mithali iyo hiyo inatumika kuielezea Israeli, yaani, wateule wa Mungu. Mungu aliwaambia Israeli: "wewe kama bibi-arusi ulinipenda mimi" (Yeremia 2:2); "Mimi ni mume wenu" (Yeremia 3:14)
Kitabu cha Ufunuo pia kinazungumza juu ya kanisa kama mwanamke
“"Ishara kuu na ya ajabu ilionekana mbinguni: mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake"”
Mwanamke huyo ame"vikwa jua". Maneno hayo yanadokeza kanisa linalong'aa kama jua, kwa sababu ya kuvikwa utukufu wa kuwako kwake Kristo. Yesu, "Nuru ya Ulimwengu" (Yohana 8:12), anaangaza kupitia kwa washiriki wa kanisa lake, nao kwa upande wao wanapaswa kuwa "nuru ya ulimwengu" (Mathayo 5:14).
Mwanamke huyo ana"mwezi chini ya miguu yake." Mwezi huo unawakilisha nuru ya Injili iliyoakisiwa [iliyoangaza] katika dhabihu na taratibu za ibada ya watu wa Mungu katika Agano la Kale. Mwezi huo ukiwa "chini ya miguu yake" unadokeza kwamba nuru ya Injili iliyoakisiwa imepitwa na huduma anayofanya Kristo.
Mwanamke huyo anayo "taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake." Nyota zinawakilisha vizuri sana mitume wale kumi na wawili, watu waadilifu ambao ushuhuda wao juu ya Yesu unang'aa sana mpaka siku hii ya leo.
Ni dhahiri, basi, kwamba maelezo yamhusuyo mwanamke huyo yanaonyesha kwamba Yohana katika mawazo yake analiona badiliko lililotokea kutoka kwa watu wa Mungu, Israeli, katika Agano la Kale kwenda kwenye kanisa lile la Kikrsto la Agano Jipya alilolianzisha Yesu. Jua, mwezi, na nyota huitilia mkazo huduma ya kupeleka nuru inayofanywa na kanisa hilo la Kikristo kwa kuzitangaza hizo Habari Njema.
