Mwokozi aliyepo daima
Masomo Yote
Sehemu 1 ya 5
SOMO 12Hatua 1 ya 5 (20%)

Mwokozi aliyepo daima

Kijana mmoja wa Kiskoti, kwa jina Petro, alipopotea katika nyika yenye majani mengi usiku mmoja uliokuwa na giza jeusi kama wino, Mungu alimwita kwa jina lake: "Petro!" Sauti ile ya mbinguni ilipoita tena, Petro alisimama katika njia yake, akaangalia chini na kugundua kwamba alikuwa umbali wa hatua moja tu kutumbukia katika shimo la machimbo ya mawe lililokuwa limeachwa.

Je! isingekuwa ni ajabu kwetu sisi kama tungeweza kumsikia Mungu akituita kwa majina yetu? Je! yasingekuwa makubwa kwetu endapo yeye angekuwa rafiki yetu aliye karibu sana nasi-endapo tungeweza kukaa pamoja naye kabisa na kuongea naye kwa muda mrefu juu ya mapambano yetu tuliyo nayo pamoja na zile ndoto zetu?

1. Kwenda Kwa Yesu Bila Kizuizi

Amini usiamini, sisi tunaweza kwenda karibu sana na Yesu sasa kuliko vile ambavyo tungeweza endapo Yeye angeishi kabisa hapa pamoja nasi akiwa ni mtu anayeonekana kwa macho. Kuwa na Yesu kimwili katika mji wetu kwa kweli lingekuwa ni jambo la ajabu, lakini hebu fikiria juu ya yale makundi makubwa sana yatakayomsonga ili yapate kumwona kwa karibu zaidi. Fikiria juu ya muda wake mwingi ambao ungetakiwa kutumika. Lingekuwa ni jambo jema kuweza kupata dakika chache za kuongea naye ana kwa ana katika kipindi chote cha maisha yetu.

Kristo anapenda kujenga uhusiano wake na kila mmoja wetu. Hii ndiyo sababu moja iliyomfanya aondoke duniani humu ili kwenda mbinguni kufanya huduma ya pekee ambayo ingemwezesha kuja karibu na kila mmoja wetu kila siku. Kwa sababu Yesu hajafungwa mahali pamoja kama alivyokuwa alipokuwa hapa duniani, yeye kwa njia ya Roho Mtakatifu sasa yuko tayari kuweza kuyaongoza maisha ya kila mtu mmoja mmoja atakaye.

Je, ni ahadi gani ya kutia moyo aliyoitoa Yesu kabla hajapaa juu kwenda mbinguni?

Mathayo 28:20
"NAMI NIPO PAMOJA NANYI SIKU ZOTE naam, mpaka mwisho wa nyakati."

Je, Kristo anafanya kazi gani kule mbinguni ambayo inafanya uwezekano uwepo kwa yeye kuwa "pamoja nanyi siku zote?"

Waebrania 4:14-16
"Basi, tuzingatie kwa makini imani tunayoungama. Maana tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia mpaka mbinguni; Yesu, Mwana wa Mungu. Huyu Mkuu wetu anaelewa kabisa unyonge wetu; yeye mwenyewe alijaribiwa kama sisi kwa kila namna lakini hakutenda dhambi. Basi, na tukikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema, tupokee huruma na neema ya kutusaidia wakati wa shida "

Zingatia ahadi hizi zinazotolewa kwetu tunapokuwa na Yesu kama mwakilishi wetu kila mmoja binafsi kule mbinguni: "Alijaribiwa kama sisi kwa kila namna." "Kutuhurumia sisi katika udhaifu wetu." "Kutusaidia wakati wa shida." Tukiwa na Yesu kama Kuhani wetu Mkuu hatuendelei tena kutanga mbali na mbingu iliyo mbali sana. Kristo anaweza kutukaribisha sisi kuingia kabisa mbele zake Mungu. Si ajabu, basi, kwamba tunaombwa sana tu "kikaribie bila hofu kiti cha enzi cha Mungu mwenye neema"

Je, Yesu anakaa mahali gani kule mbinguni?

Waebrania 10:12
"Lakini Kristo alitoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi milele dhabihu ifaayo kisha akaketi UPANDE KULIA WA MUNGU"

Kristo aliye hai-mmoja anayetuelewa sisi-ni mwakilishi wetu kila mmoja binafsi katika kiti kile cha enzi "mkono wa kuume wa Mungu."

Ni kwa jinsi gani maisha ya Yesu yalimwandaa kuwa Kuhani wetu?

Waebrania 2:17,18
"Ndiyo maana ilimbidi awe kama ndugu zake wa kila namna, ili awe Kuhani Mkuu wao aliye mwaminifu na mwenye huruma katika kumtumikia Mungu, ili dhambi za watu ziondolewe. Na, anaweza sasa kuwasaidia wale wanaojaribiwa na kuteswa"

"Ndugu" yetu aliyeshiriki katika ubinadamu wetu, na ambaye "alijaribiwa" kama sisi tunavyojaribiwa, hivi sasa yeye ni Kuhani wetu Mkuu ameketi upande wa kulia wa Mungu, "Alifanywa kama" sisi, anajua yale tunayoyapitia. Amepata kuwa na njaa, kiu, majaribu, na kuchoka sana kiasi cha kuishiwa nguvu. Alijisikia kwamba alikuwa na haja ya kuhurumiwa na kueweleka.

Lakini zaidi ya hayo yote, Yesu anazo sifa za kuwa Kuhani wetu Mkuu kwa sababu yeye alikufa ili "kufanya upatanisho" kwa ajili ya dhambi zetu. Alilipa gharama yote ya dhambi zetu kwa kufa badala yetu sisi. Hii ndiyo Injili, yaani, Habari Njema kwa wanadamu wote kila mahali na kwa wakati wote.

Mmojawapo wa Wakurugenzi wa Shule yetu ya Biblia anatusimulia kisa hiki kilichompata akisema "Binti yetu mdogo kabisa alipokuwa na umri wa miaka mitatu, alijibana kidole chake katika kiti cha kukunjwa, na kuuvunjavunja mfupa wake. Tulipomkimbiza kumpeleka kwa daktari, kilio chake kikali kutokana na maumivu yake kiliturarua kweli mioyo yetu. Tena kikamgusa mtoto wetu wa miaka mitano kwa njia ya pekee. Sitaweza kusahau maneno yake aliyosema baada ya daktari kumshughulikia dada yake aliyejeruhiwa. Binti yule akalia kwa kwikwi, na kusema, 'Baba, natamani kingekuwa ni kidole changu mimi!"

Wanadamu wote waliposetwa na dhambi na kuhukumiwa kufa milele, Yesu alisema, "Baba, natamani ningekuwa mimi." Naye baba akampa Yesu kile alichotamani pale msalabani. Mwokozi wetu amepitia kila aina ya maumivu makali ambayo kwayo sisi tuliteseka - na zaidi ya hayo!