Mapema katika miaka ile ya kuanzia 1960 na kuendelea, Ndugu Andrew, mtu wa Uholanzi, aliingiza kwa siri mzigo wa Biblia katika gari lake la Volks Wagen (Folks Vageni) na kuvuka mpaka wa Romania na kuwapita walinzi wa kikomunisti. Alipanga katika hoteli moja na kuanza kuomba kwamba Mungu amwongoze kwenda kwenye makundi ya Kikristo yanayofaa - yaani wale ambao wangeweza kuzitumia vizuri sana zile nakala zake za Maandiko.
Mwisho wa juma lile Andrew alitembea kwenda kwa karani wa hoteli ile na kumwuliza angeweza kulipata wapi kanisa.
Yule karani akamwangalia kwa njia isiyo ya kawaida kidogo na kujibu, "Hatunayo mengi ya hayo, unajua. Isitoshe, usingeweza kuielewa lugha yetu"
"Je! Wewe hukujua?" akajibu Andrew, "ya kuwa Wakristo wanazungumza lugha ya ulimwengu mzima."
"Ehee! Ni lugha gani hiyo?"
"Inaitwa Agape [Upendo]"
Yule karani alikuwa hajapata kuisikia kamwe, lakini Andrew alimhakikishia kwa kusema hivi, "Ni lugha nzuri kuliko zote ulimwenguni"
Andrew aliweza kuyapata makundi kadhaa ya kanisa katika eneo lile na kufanikiwa kupanga kuonana na mwenyekiti na katibu wa dhehebu fulani. Kwa bahati mbaya, ingawa Andrew na watu hao walijua lugha kadhaa za Ulaya, wakajikuta hawana lugha hata moja waliyoijua wote. Basi, wakakaa pale wakikodoleana macho tu. Andrew alikuwa amesafiri maili nyingi za hatari na ule mzigo wake wathamani, lakini ikaonekana ya kwamba hapakuwa na njia yoyote ya kujua iwapo watu wale walikuwa ni ndugu Wakristo wa kweli au makachero wa Serikali.
Hatimaye akaiona Biblia ya Kiroma juu ya meza katika ofisi ile. Andrew akaingiza mkono wake katika mfuko wake na kuichomoa Biblia ya Kiholanzi. Alifunua 1 Wakorintho 16:20, na kuishika Biblia akiwa amenyosha mkono wake akisonda kidole chake kwenye jina la Kitabu kile waliweza kulitambua. Mara moja nyuso zao zikang'aa kwa meru. Upesi wakaipata sura ile ile na fungu lile lile katika Biblia zao za Kiromania, Kisha wakasoma maneno haya: "Ndugu wote hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu."
Watu wale wakatabasamu na kumwangalia Andrew. Kisha mmoja wao akapekua katika Biblia yake na kupata Mithali 25:25. Andrew akalipata fungu lile na kulisoma "kama vile maji baridi yalivyo kwa mtu mwenye kiu, ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali "
Watu wale walitumia nusu saa wakiongea na kupeana habari - kwa kupitia tu katika maneno ya Maandiko. Walikuwa na furaha nyingi sana kwa urafiki wao huo uliovuka mipaka yote ya utamaduni hata wakacheka mpaka machozi yalipowatoka.
Andrew alijua kwamba amewapata ndugu zake. Alipowaonyesha mzigo wake wa Biblia, Waromania wale walitekwa nao wakamkumbatia tena na tena.
Jioni ile katika ile hoteli, yule karani alikuja karibu na Andrew na kusema kwa mshangao, 'Aisee, nilitafuta 'agape' katika kamusi. Hakuna lugha ya jina lile. Hilo ni neno la Kigiriki limaanishalo upendo.
Andrew akajibu "sawasawa. Mimi nilikuwa nazungumza kwa kutumia neno hilo mchana kutwa".
Je! Wewe umeigundua lugha hiyo nzuri? Katika mwongozo huu utajifunza juu ya jinsi Mungu anavyoweza kutuleta sisi sote katika jamii yake kubwa ya upendo.
