Larry alikuwa akifurahia maongozi yale mazuri, chai ya kijapani, wali mkavu, nyumbani kwa Bwana Komari wakati wageni wengine walipoanza kuzitoa Biblia zao. Wote wakamtazama na kumngojea. "Tafadhali tupe somo letu sasa?" Bwana Komari aliomba.
Larry alikuwa karibu amepaliwa na chai yake. Alikuwa amedhani kwamba mkutano ule wa dhifa (Karamu) ulikuwa wa kujifurahisha tu. Na sasa hakuweza kufikiri juu ya kitu chochote cha kusema.
Kwa kweli Larry alikuwa amefundisha madarasa mengi ya Biblia katika shule ya Kikrsito ya Lugha ya Kiingereza katika nchi ya Japan alikokuwa akifanya kazi. Lakini yalikuwa yameandaliwa vizuri. Aliweza kutoa maelezo juu ya Biblia kwa wepesi. Lakini kuweza kuzungumza habari za Mungu papo hapo bila kujiandaa vizuri… hilo lilikuwa ni jambo tofauti.
Larry alikuwa amezisikia hadithi zote za Biblia tangu utoto wake. Lakini hazikuwa na maana sana kwake kwa msingi wa kibinafsi. Alikuwa anafanya mambo aliyojua kwamba yalikuwa mabaya machoni pake Mungu. Angewezaje basi, kuwaambia wengine habari za Mungu ambaye yeye mwenyewe alikuwa hamjui kwa kweli?
Basi, akiwa ameketi pale kwenye kochi lile, amezungukwa na watu waliokuwa wakimngojea, mchezo wake wa viigizo bubu ulikuwa karibu kuporomoka. Katika saa ile ya hofu yake, fungu likapita kasi mawazoni mwake lililosema kwamba roho Mtakatifu aweza kutupa sisi maneno ya kusema tunapoletwa mbele ya watu kutoa ushuhuda wetu (Luka 12:12). Alitoa sala yake ya kufa na kupona kuomba msaada, kisha akaking'ang'ania kisa kile kinachojulikana sana ambacho aliweza kukifikiria: yaani, kisa cha mwana mpotevu.
Alipoeleza jinsi Mungu anavyowapenda sana hata wale ambao wanatangatanga mbali naye, Larry akajikuta anaongea moja kwa moja toka moyoni mwake. Maneno yake yalikuwa yakiwaingia wale watu. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake Larry alitambua jinsi Mungu alivyompenda sana.
Usiku ule Larry alipiga magoti kando ya Kitanda chake na kutoa maisha yake kwa Mungu ambaye hatimaye alikuwa ni wa kweli kwake. Kushuhudia juu ya upendo wa Mungu kulifanya jambo hilo kuwa zaidi ya jambo la kawaida la kuwazia tu. Sasa likawa ni jambo la kweli lililomshinda nguvu.
