Hapakuwa na alama zo zote za vidole. Hakuna silaha yo yote iliyogunduliwa. Hakuna mtu ye yote aliyemwona mwuaji yule alipoingia katika ofisi ya yule daktari. Hakuna ye yote aliyesikia hata zilipofyatuliwa zile risasi. Lakini yule daktari alikuwa na risasi tano zimepenya shati yake.
Ilionekana kana kwamba ni uhalifu uliofanywa kwa ustadi sana. Mwanzoni Polisi hawakuweza kupata vidokezo vyo vyote. Lakini halafu waliona waya mwembamba sana uliofungwa kwenye chombo cha kuwekea kalamu ya risasi juu ya meza ya daktari yule. Waya ule ulikwenda kwenye kinasa sauti (tepurekoda) kilichokuwa ndani ya mtoto wa meza. Chombo kile cha kuwekea kalamu ya risasi, wakang'amua, kilificha hasa ile maikrofoni aliyoitumia yule daktari kuweka kumbukumbu ya mazungumzo yake na wagonjwa aliokuwa akiwapa ushauri.
Wapelelezi waliirudisha nyuma ile tepu ya kurekodia sauti, na kwa mshangao wao, wakaanza kuisikiliza ile tepu ilipofunguliwa tena kuhusiana na uhalifu ule wenyewe. Mtu aliyeitwa Antoni alikuwa ameingia katika ofisi ile na kuanza mabishano makali na yule daktari. Risasi zikafyatuliwa. Tepu ile iliishia na sauti ya maumivu makali ya daktari yule, aliyekuwa akifa juu ya lile zulia.
Kila habari ndogo ndogo ya kuogofya ilikuwa imerekodiwa. Yule mwuaji alidhani kwamba uhalifu wake ule ungebaki kuwa siri milele. Alikuwa mwangalifu sana kutokuacha kidokezo cho chote. Lakini ile tepu ilisimulia kisa chote.
Katika mwongozo huu tutajifunza habari za hukumu ya mwisho ya Mungu wakati wanadamu wanaendelea "kuhukumiwa sawa sawa na matendo yao kama yalivyorekodiwa katika vitabu vile" (Ufunuo 20:12). Kwa wale ambao hawajampokea Kristo kama Mwokozi wao, itakuwa ni habari mbaya kwao. Lakini hukumu hiyo ni habari njema za ajabu kwa wale walioupata usalama wao ndani yake Kristo.
