Mabaharia waasi maarufu walioizamisha meli ya Kiingereza iliyoitwa Bounty waliishia kufanya makazi yao wakiwa pamoja na wanawake, wenyeji wa eneo lile katika kisiwa cha Pitcairn katika Bahari ya Pasifiki ya Kusini. Kundi lile lilikuwa mabaharia tisa wa Kiingereza, wanaume wa Kitahiti sita, wanawake wa Kitahiti kumi, na msichana wa miaka kumi na mitano. Mmojawapo wa mabaharia wale alivumbua namna ya kutonesha [kugeuza kuwa mvuke] alkoholi, na baada ya muda mfupi ulevi ukaliharibu koloni lile lililokuwa katika kisiwa kile. Ugomvi kati ya wanaume na wanawake ukageuka na kuwa wa kutumia nguvu.
Baada ya kupita muda fulani mmoja tu kati ya wanaume wale wa kwanza waliofika mle kisiwani ndiye alibaki kuwa hai. Lakini mtu huyo, Alexander Smith, alikuwa ameigundua Biblia katika mojawapo la makasha yaliyochukuliwa kutoka katika ile meli. Alianza kuisoma na kuwafundisha wengine juu ya kile ilichosema. Alipofanya hivyo maisha yake yeye mwenyewe yakabadilika na hatimaye maisha ya wote waliokuwa katika kisiwa kile.
Je, hivi Mungu bado anaendelea kusema na watu kupitia katika kurasa hizo za Biblia? Bila shaka anafanya hivyo. Ninapoandika haya, naliangalia karatasi la majibu lililotumwa kwetu na mwanafunzi mmojawapo wa kozi zetu za Biblia. Maelezo chini yake yanasema hivi "Mimi nimo gerezani, niko katika orodha ya watu wanaostahili kunyongwa, nimehukumiwa kufa kwa kutenda kosa la jinai. Kabla ya kuchukua kozi hii ya Biblia, nilikuwa nimepotea lakini sasa ninacho kitu cha kutumainia tena nimeupata upendo mpya."
Biblia inao uwezo unaoweza kuyabadilisha kabisa maisha ya watu. Kwa kweli, watu wanapoanza kujifunza Biblia, maisha yao hubadilika kwa namna ya kuvutia sana.
