Katika mwaka ule wa 1929 (Frank Morris) alipanda meli iliyokuwa ikienda Uswisi. Alikuwa ametazamia kufanya safari ile kwa muda fulani. Lakini ikageuka na kuwa safari ya kumdhalilisha. Mtumishi aliyewekwa kumtunza alimfungia Frank katika chumba chake kila siku. Baada ya kupata kifungua kinywa, kwa haraka-haraka Frank aliweza kufanya mazoezi ya viungo kidogo, lakini yeye alijisikia kana kwamba alikuwa mpumbavu kuweza kuongozwa vile huku na huku juu ya sitaha ya meli ile, kama vile yeye alikuwa mnyama anayeongozwa kwa kamba. Wakati wo wote alipokutana na abiria aliyeonyesha urafiki kwake na kumwalika kwenda kutembea naye, yule mtumishi alikataa, akawaambia kwamba alipaswa kumwangalia kila wakati.
Frank alikuwa mtu mzima, mwenye hisia za kawaida za udadisi na tamaa anazopaswa kuwa nazo mtu mzima. Lakini yeye alikuwa kipofu pia. Yule mtumishi alidhani kwamba asingeweza kujitunza mwenyewe. Frank alitendewa kana kwamba alikuwa kifurushi vile, kilichopaswa kuburutwa huku na huku.
Lakini katika nchi ile ya Uswisi maisha ya Frank yalibadilika kwa namna ya kuvutia sana. Alipokuwa kule alijifunza habari za mbwa waliokuwa wamepewa mafunzo ya kuwaongoza vipofu. Aliporudi kule Marekani pamoja na kiongozi [mbwa] wake wa safari wa Kijerumani aliyeitwa Buddy, Frank alianzisha Jicho Lionalo, sasa ni shirika lililoenea ulimwenguni kote.
Sasa Frank, akiwa na Buddy kando yake, aliweza kwenda ko kote, wakati wo wote, na mtu ye yote. Hatimaye alijisikia huru. Katika maonyesho yake ya kwanza kwa waandishi wa habari penye njia panda yenye magari mengi katika lile Jiji la New York, yule Buddy alimwongoza bwana wake kwa ustadi kutoka katika njia moja na kuingia katika njia nyingine wakati yale magari yalipokuwa yakiunguruma na kupita. Kwa kuwa yeye alimtumainia yule Buddy, Frank alivuka kwa urahisi mpaka upande ule wa pili. Waandishi wa habari walioonekana pale walikuwa na wakati mgumu zaidi kuvuka pale; mmoja wao alichukua kabisa teksi ili kwenda upande ule wa pili.
Katika kurasa chache zifuatazo tunakwenda kujifunza juu ya Roho Mtakatifu, kiongozi anayetaka sisi tuyakabidhi maisha yetu mikononi mwake. Sisi sote tumelemaa kutokana na asili yetu moja ya kibinadamu, tunao upofu ule ule katika mambo yale yaliyo ya maana sana kwetu. Maisha yetu hupita kasi kwa namna ambayo tunajikuta wenyewe tunayavumilia tu badala ya kwenda mahali fulani. Hata hivyo, sisi tunasita-sita kuyakabidhi maisha yetu kikamilifu kwa Kiongozi huyo. Lakini ugunduzi unaomngojea kila mmoja wetu ni huu: sisi tutapata uhuru wa kweli na uwezo kwa kumtegemea Roho Mtakatifu kutuongoza katika maisha yetu yote.
